Kwa mwenendo huu, michezo haitafanikiwa Tanzania
Mama Anna Kibira / Mwenyekiti wa Chama cha Netboli Taifa(CHANETA) |
Chama cha Netiboli Tanzania (Chaneta) kilitangaza
kuiondoa timu hiyo kutokana na kukosa fedha za gabarone, Botswana
kushiriki mashindano ya Afrika ya kutafuta tiketi ya kwenda Kombe la
Dunia.
Huenda kwa mara ya kwanza tungeshuhudia Taifa
Queens ikikata tiketi ya kushiriki michuano hiyo mikubwa, lakini ndoto
hizo ziliyeyushwa na Chaneta.
Chaneta ilitembeza bakuli la kutafuta fedha za
kufanikisha safari hiyo, lakini haikufanikiwa. Kushindwa kwa Taifa
Queens kwenda kwenye mashindano hayo ni mwendelezo wa timu za Taifa
kukosa mashindano muhimu.
Shirikisho la Riadha Tanzania (RT) pia limekuwa
likijiendesha kwa mtindo huo, hali kadhalika kwa vyama vya ngumi,
kikapu, mpira wa meza, judo na vingine vingi. Utaratibu huo wa kutembeza bakuli unaotumiwa na
vyama umekuwa ukididimiza michezo yetu kimataifa na waathirika wakubwa
katika hilo wakiwa wachezaji.
Tumekuwa tukishuhudia mataifa mengine yakipata
mafanikio katika sekta ya michezo siyo kwa kutumia mtindo wa kutembeza
bakuli bali mifumo mizuri ya udhamini na vyanzo vya uhakika vya mapato. Hapa nchini ni dhahiri Serikali imejiondoa
kusaidia michezo, kwani hutenga fedha kidogo sana katika bajeti ya
maendeleo ya michezo, pia hutoa mchango mdogo kwa timu za taifa.
Matukio ya timu za taifa kujiondoa kwenye
mashindano ya kimataifa yamekuwa ya kawaida, hakuna anayehoji wala
anayetafakari ni kiasi gani Tanzania inazidi kupoteza dira katika nyanja
ya michezo kimataifa.
Kila siku sera za viongozi wa vyama na
mashirikisho haya ya michezo ni kulalamika. Hakuna chama wala shirikisho
lenye afadhali kimapato ambalo linaweza kujiendesha.
Asilimia 95 ya vyama na mashirikisho ya michezo
hapa nchini hayana vyanzo vyake vya mapato vya kueleweka. Karibu vyote
vinajiendesha kwa kutembeza bakuli. Mtindo huu umekuwa ukididimiza maendeleo ya
michezo kwani timu ya taifa ya ngumi ilikwama kushiriki kwenye
mashindano ya Afrika nchini Morocco, pia riadha nayo ilikwama kabla ya
netiboli kukwama baada ya vyama vya michezo hiyo kutembeza bakuli bila
mafanikio.
Tabia hii ya kutembeza bakuli imeanza kuigharimu Tanzania kwani
tumeshuhudia timu ya netiboli ikizidi kuporomoka na sasa imezidiwa hadi
na Uganda kwenye viwango vya kimataifa. Serikali ilipojitoa kusaidia michezo moja kwa
moja, nilitegemea wangeiacha katika misingi mizuri ya kujiendesha,
lakini cha kushangaza utaratibu wa michezo uliotumika miaka 30 iliyopita
ulikuwa bora kushinda sasa.
Niliwahi kuzungumza na baadhi ya wanamichezo wa
zamani ambao walionyesha kustaajabu mfumo hasi unaotumika hivi sasa
kulinganisha na miaka ya 70 mpaka 80. Wanamichezo hao wa zamani waliniambia Taifa
halikuwa na utaratibu wa kutembeza bakuli. Michezo iliwekwa katika
bajeti za Serikali na mafanikio yalionekana ambayo hivi sasa yamebaki
historia.
Hakuna njia ya mkato ya kufanikiwa katika michezo
bali ni vyama kuwa na vyanzo vyake vya mapato au udhamini wa kudumu kwa
timu zao, ikiwezekana Serikali kuingilia kati.
Kwa mtindo huu wa kutembeza bakuli hatuwezi kufanikiwa katika sekta ya michezo kimataifa zaidi ya kuwa wasindikizaji. Mwandishi wa uchambuzi huu ni mwandishi wa habari wa habari wa gazeti hili.
CHANZO: Mwananchi
Comments
Post a Comment