Malinzi maji ya shingo
Jamal Malinzi / Rais wa Shirikisho la Mpira Tanzania (TFF) |
Hayo yamesemwa jana jijini Dar es Salaam na wakili wa kujitegemea Dk. Damas Ndumbaro, anayeiwakilisha TPL Board na klabu 14 za Ligi Kuu, katika jaribio lao la kupinga shinikizo la TFF kuzikata klabu hizo asilimia tano ya pesa za wadhamini wa ligi hiyo ambao ni Kampuni ya Vodacom na Azam Media Ltd.
Uamuzi huo wa TPL Board na klabu za Ligi Kuu, umekuja siku moja baada ya Malinzi kusisitiza kuwa uamuzi wa kukata asilimia tano ya makato ya pesa za wadhamni kwa klabu za ligi hiyo uko palepale, na kwamba bodi hiyo haina mamlaka ya kupinga agizo hilo na wenye uwezo au mamlaka hayo ni Kamati ya Utendaji ya TFF.
Akijibu hoja moja baada ya nyingine kama alivyoelekezwa na wateja wake, Dk. Ndumbaro alisema kuwa bodi na klabu zinakiri na kutambua kwamba TPL Board ni zao la Mkutano Mkuu wa TFF, lakini kitendo cha Malinzi kuingiza mabadiliko ya kanuni na sheria bila Mkutano Mkuu ni ukiukwaji wa katiba.
Hiyo inazilazimisha klabu kutishia kugomea ushiriki wa Ligi Kuu, ikiwamo kutovaa jezi za mdhamini Vodacom na kutoruhusu mechi zake kuoneshwa na Azam Tv iwapo zitakatwa kilazima, huku mchakato wa kusaka saini za Wajumbe wa Mkutano Mkuu ukitarajia kuanza mapema wiki ijayo.
“Klabu zimenitaka kuandaa waraka wa kuomba Mkutano Mkuu wa Dharura wa TFF, ambao kwa kawaida unaitishwa kwa kupata theluthi mbili za saini za wajumbe. Lengo kuu la mkutano huo litakuwa ni kupiga kura ya kutokuwa na imani na Rais wa TFF na kuweka bayana dhuluma inayofanywa na TFF,” alisema Ndumbaro.
Katika hoja namba tatu ya Malinzi aliyoitoa juzi, alisema: “Kisheria Bodi ya Ligi sio chombo huru (its not a legal entity), hivyo Bodi pamoja na mambo mengine haina mamlaka ya kuingia mikataba ya aina yoyote ya kisheria,” hoja iliyopingwa na Ndumbaro kwa kuonesha saini ya Silas Mwakibinga katika mkataba na Azam Media.
“Anachofanya Malinzi ni kukiuka katiba. Saini katika mkataba wa Azam Media hii imesainiwa na Mwakibinga ambaye ni Ofisa Mtendaji Mkuu, huo uhalali wa TPL Board kuingia mkataba umeletwa sasa?
Huko ni kunyimana uhuru, kwa sababu kama wanadhani bodi haina ‘legal entity’, klabu za Ligi Kuu zinazo ‘legal entity’,” alisisitiza.
Klabu hizo kupitia Ndumbaro zimesisitiza kuwa, zitauomba Mkutano Mkuu wa Dharura kuiwajibisha Kamati ya Utendaji ya TFF, ambayo imeingilia maamuzi ya awali ya Mkutano Mkuu uliounda Bodi ya Ligi, kwani tangu Malinzi aingie madarakani Oktoba mwaka jana, hajawahi kuitisha Mkutano Mkuu.
Ndumbaro alisema, kitendo cha kuingiza kanuni ama sheria ya makato, ni kwenda kinyume na Mkutano Mkuu uliozaa Bodi ya Ligi na kwamba TFF inapaswa kufika mahali ikaona aibu kwa aina ya unyonyaji inaoufanya kwa klabu ambazo zinapata pesa ndogo katika mikataba hiyo kuliko shirikisho hilo.
Akichanganua mapato ya udhamini kwa klabu na TFF, Ndumbaro alisema wakati kila klabu ilipata kiasi cha sh. Mil. 100 kwa msimu wa kwanza, mil. 110 msimu wa pili na mil. 121 katika msimu wa tatu kwa mkataba wa Haki za Matangazo ya Tv; TFF imejikusanyia sh. Mil.140 kwa msimu wa kwanza, mil. 154 wa pili na mil. 169 wa tatu.
“Hiyo ndio kusema kuwa, wakati kila klabu ikitarajia kupata sh. Mil. 331 katika misimu mitatu ya mkataba wa Azam Tv, TFF itajikusanyia sh. Mil 463, hiyo ni mbali ya mil. 516 inazopata katika gawio la mkataba wa Vodacom.
Huu kama si uonevu ni nini wakati klabu ndizo zinazomiliki timu za vijana?” alihoji Ndumbaro.
Katika jaribio lake la kukata asilimia tano ya pesa za klabu kwa kila mdhamini miongni mwa wadhamini wawili wa Ligi Kuu, Malinzi alisema nia ni kuunda Mfuko Maalum wa Kuendeleza Soka la Vijana, ambao utakuwa chombo maalum kwa ajili ya kukusanya fedha toka vyanzo mbali mbali kwa ajili ya kuendeleza miradi ya soka la vijana nchini.
Ndumbaro aliitaka TFF kutumia pato la viingilio linalokwenda kwa Mfuko wa Maendeleo ya Soka (FDF), kuliko kuzinyonya klabu ambazo zina vikosi vya timu za vijana ambazo zinategemea pato hilo hilo la klabu za Ligi Kuu ili kuziwezesha kukabiliana na majukumu mengine.
“Wakati Malinzi akiwania madaraka ya kuingia TFF, alikuwa akiahidi kutafuta wadhamini wa kunyanyua soka la vijana, anapaswa kuongeza bidii katika kuwatafuta wadhamini hao na si kuzinyonya klabu, ambazo kimsingi zina mzigo mkubwa wa majukumu ya kutunza timu zao za vijana ambazo hazina wadhamini,” alisisitiza Ndumbaro.
Ndumbaro ameitaka serikali kutuma Mkaguzi wa Hesabu za Serikali kukagua hesabu za TFF, ili kuona namna shirikisho hilo linavyopokea na kutumia pesa kutoka vyanzo vyake, ambako itakutana na ufujaji.
Alibainisha kuwa, katika suala zima la viingilio, TFF imekuwa ikikata shilingi 1,000 katika kila tiketi ya Ligi Kuu inayouzwa, makato yanayofanyika kabla ya kuhesabu mapato ya jumla ya kila mchezo, hivyo kuinyima serikali kupitia TRA mapato, lakini pia kuwanyonya wamiliki wa viwanja na klabu husika.
“Msimu uliopita zaidi ya tiketi 700,000 ziliuzwa, hivyo walijikusanyia zaidi ya sh. Mil. 700 na msimu huu matarajio ni kuuza tiketi zaidi ya milioni moja ambako watapata zaidi ya shilingi bilioni moja, ambazo wanapaswa kuzitumia hizo katika kukabili majukumu yao,” alisisitiza Ndumbaro wa Kampuni ya Ndumbaro and Maleta Advocates.
Alimaliza kwa kumtaka Malinzi na TFF kukaa mezani na wateja wake kujadili suala moja baada ya jingine, vinginevyo wataendelea na mchakato wa kusaka theluthi mbili za saini za Wajumbe wa Mkutano Mkuu, ambao utakapoitishwa, watautumia kupiga kura ya kutokuwa na imani na Malinzi aliyeingia madarakani.
CHANZO: Tanzania Daima
Comments
Post a Comment