Tathmini ya Madola, ifanyiwe kazi
Timu ya Tanzania kwenye michezo ya Jumuiya ya Madola yakaribishwa rasmi leo katika kijiji maalum cha michezo hiyo Glasgow |
Kwa mara ya kwanza katika historia ya Tanzania, Serikali
ilikutana na wanamichezo kwa ajili ya kufanya tathmini ya ushiriki wa
taifa kwenye michezo ya Jumuiya ya Madola ya 2014 ambayo Tanzania
ilitoka kapa kwa mara ya pili mfululizo.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa
Kimataifa, Bernard Membe ndiye alikuwa mgeni rasmi katika tathmini hiyo
iliyowahusisha wachezaji, makocha na viongozi wa vyama mbalimbali vya
michezo.
Katika tathmini hiyo, vyama vililalamikiwa kutokuwa makini katika kuziandaa timu zao kwa ajili ya mashindano ya kimataifa.
Maandalizi duni ilikuwa ni moja ya sababu kubwa
iliyotajwa katika tathmini hiyo iliyohusisha wanamichezo wa ngumi,
riadha, mpira wa meza, judo, kuogelea, baiskeli na kunyanyua vitu vizito
walioiwakilisha nchi katika michezo ya madola iliyofanyika Scotland.
Maandalizi ya zimamoto ni ugonjwa sugu ulio kwenye
timu za Tanzania, baada ya tathmini ya madola nilitegemea vyama
vingeanza kujipanga na kujiandaa kwa ajili ya michezo ya Afrika ya 2015.
Baada ya tathmini ile kila chama kimeshika njia
yake, hakuna kinachokumbuka kufanya maandalizi ya kina kama ambavyo
vilieleza katika tathmini ya Madola.
Mataifa ya Afrika yanayofanya vizuri katika
michezo tayari yameanza maandalizi kwa ajili ya michezo ya Afrika,
tofauti na Tanzania ambayo imekuwa na rekodi mbaya kwenye michezo
kimataifa na hakuna chama kinachokumbuka maandalizi.
Licha ya kwamba Waziri Membe aliahidi kufanya
jitihada kuhakikisha aibu ya madola haijirudii kwenye michezo ya Afrika,
bado jitihada hizo zinapaswa kuungwa mkono na vyama vya michezo. Baada ya kumalizika michezo ya Madola nilitegemea
vyama vingejifunza kutokana na makosa, vingetambua umuhimu wa mazoezi
hatua baada ya hatua na mchakato hadi mchezaji kushinda medali.
Imekuwa kinyume, vyama sasa viko likizo vinaona
2015 ni mbali, vimekaa vikisubiri miezi miwili kabla ya mashindano ndipo
vianze maandalizi. Imefikia hatua sasa Watanzania wamezichoka timu zao,
wanapoteza imani nazo kila zinapokuwa kwenye mashindano ya kimataifa.
Ubabaishaji wa viongozi wetu wa michezo ndiyo chanzo, viongozi wetu wanapenda mtelemko katika maandalizi.
Tulishuhudia wakati timu zikichaguliwa kwenda
kwenye kambi nje ya nchi iliyoandaliwa na serikali kabla ya michezo ya
madola kufanyika, viongozi wa vyama walikuwa mstari wa mbele kuchuja
wachezaji na kujipendekeza kuwa makocha.
Japo wamekuwa wa mwisho kuweka mikakati ya kutafuta fedha kwa
ajili ya kuziandaa kwa kina timu zao ili kuhakikisha zinafanya vizuri
kimataifa. Tena cha kushangaza hao hao viongozi waliofanya
kampeni kisha kupigiwa kura ili kuongoza vyama na mashirikisho yetu ya
michezo ndiyo wanakuwa mstari wa mbele kusema maandalizi hayakuwa
mazuri.
Kama kiongozi anasema maandalizi hayakuwa mazuri
alitegemea muujiza gani ushuke kwa ajili ya kuratibu maandalizi ya
wanamichezo wa chama anachokiongoza?. Kama vyama vya michezo vikishindwa kubadilisha
mifumo yao ya maandalizi kwa wanamichezo hakuna shaka hata kwenye
michezo ya Afrika 2015 hali itakuwa ileile kwa Tanzania.
Kama kweli Taifa linahitaji mafanikio, viongozi wa
vyama vya michezo wangezifanyia kazi kasoro zote zilizoainishwa na
wachezaji wakati wa ufanyaji tathmini vinginevyo taifa litaendelea
kutwanga maji kwenye kinu katika michezo kimataifa.
Mwandishi wa uchambuzi huu ni mwandishi wa habari wa gazeti hili.
CHANZO: Mwananchi
CHANZO: Mwananchi
Comments
Post a Comment